Bunge la Sierra Leone limeidhinisha mageuzi ya kikatiba yatakayobadilisha sheria za uchaguzi nchini humo kabla kinyang'anyiro cha kuwania urais kuanza. Taifa hilo la Afrika Magharibi litafanya uchaguzi mwaka 2028.
Spika wa bunge Segepoh Solomon Thomas alisema baada ya kikao kuwa muswada huo ulioungwa mkono na chama tawala cha Sierra Leone Peoples, SLPP uliidhinishwa kwa zaidi ya nusu ya wabunge waliopiga kura. Hata hivyo idadi ya kura haikutangazwa.
Wabunge wa chama kikuu cha upinzani cha All People's Congress APC walitoka nje baada ya kushindwa kulishawishi bunge kwamba mageuzi hayo yalihitaji wingi wa theluthi mbili.
Mabadiliko hayo yangepunguza kiwango cha kura kinachohitajika kushinda urais kutoka asilimia 55 hadi zaidi ya nusu ya waliopiga kura kitaifa, huku yakianzisha mfumo wa uwakilishi wa uwiano katika uchaguzi wa wabunge.