RAIS DKT. MWINYI: TAMASHA LA KIZIMKAZI LIMEENDELEA KUFUNGUA FURSA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Tamasha la Kizimkazi limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutangaza utamaduni, utalii, biashara na fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar, sambamba na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 12 Agosti 2026, alipozindua rasmi Tamasha la Kizimkazi 2026, Mkoa wa Kusini Unguja, lenye kaulimbiu “KIZIMKAZI Kumenoga!”

Rais Dkt. Mwinyi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono ya kuasisi Tamasha la Kizimkazi, ambalo limeendelea kukuza na kuhifadhi mila na utamaduni pamoja na kuchochea maendeleo ya wananchi wa Kizimkazi na Mkoa wa Kusini Unguja kwa ujumla.

Rais Dkt. Mwinyi amepongeza ubunifu unaoendelea kuongezwa katika Tamasha hilo kupitia shughuli mbalimbali, yakiwemo mashindano ya ngalawa, maonesho ya sanaa, michezo, vyakula vya asili, muziki, maonesho ya biashara na uzinduzi wa miradi ya maendeleo. Amesema shughuli hizo zina mchango katika kuenzi utamaduni, kuutambulisha kwa vizazi vijavyo na kuongeza mvuto wa Tamasha.

Aidha, amesema Tamasha hilo limekuwa jukwaa la kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia maonesho ya biashara, miradi ya maendeleo na makongamano mbalimbali, yakiwemo yanayohusu matumizi ya nishati safi pamoja na fursa zinazopatikana katika Uchumi wa Buluu.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Tamasha la Kizimkazi linaunga mkono dhamira ya Serikali ya kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar kutoka 800,000 hadi kufikia milioni 1.5, kwa kuongeza matukio maalum ya utalii na kuendelea kutangaza vivutio vya asili, urithi wa kihistoria, utamaduni, vyakula na ukarimu wa Wazanzibari.

Akizungumzia fursa za Mkoa wa Kusini Unguja, Rais Dkt. Mwinyi ameutaka uongozi wa Mkoa na Wilaya zake kuendelea kutumia Tamasha hilo kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika ardhi na bahari, ili rasilimali hizo ziweze kuongeza tija na manufaa kwa wananchi.

Amesema Serikali imejizatiti kuendeleza sekta ya uvuvi kwa kuimarisha miundombinu, ikiwemo ujenzi wa madiko ya kisasa, masoko bora na bandari za uvuvi, sambamba na kuhamasisha uvuvi wa bahari kuu kwa kutumia zana na vyombo vya kisasa ili kuongeza uzalishaji na kipato cha wavuvi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema bado ipo fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa aina za mwani zinazohitajika katika masoko ya dunia pamoja na kuongeza thamani ya zao hilo, ili wakulima waweze kupata manufaa makubwa zaidi.

Rais Dkt. Mwinyi pia amepongeza mchango wa Sekta Binafsi katika maendeleo ya Mkoa wa Kusini Unguja, hususan uwekezaji katika hoteli za kitalii, ambao umechangia kuongeza ajira, mapato ya Serikali na fursa za kiuchumi kwa wananchi. Ameihakikishia Sekta Binafsi kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, hasa katika sekta za utalii, viwanda na Uchumi wa Buluu.

Kabla ya uzinduzi huo, Rais Dkt. Mwinyi, akiwa na Mkewe Mhe. Mama Mariam Mwinyi, viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi wameshiriki matembezi kuanzia Kibuteni hadi Kizimkazi pamoja na mazoezi ya viungo.

Baadaye, Rais Dkt. Mwinyi amekagua mabanda mbalimbali ya maonesho yaliyoshirikisha taasisi za Serikali, Sekta Binafsi, wafanyabiashara na wajasiriamali, na kujionea bidhaa, huduma pamoja na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na wadau hao.

Dkt. Mwinyi ameipongeza Kamati ya Maandalizi, wadhamini, taasisi za Serikali, Sekta Binafsi, wajasiriamali, wasanii, wanamichezo na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja kwa ushiriki wao katika kufanikisha Tamasha la Kizimkazi 2026, na kuhimiza kuendelea kulitumia Tamasha hilo kufungua fursa mpya za maendeleo kwa wananchi.

Katika mwendelezo wa matukio ya Tamasha la Kizimkazi, Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kufungua mradi mpya wa makaazi wa Amani Residency na kushiriki Hafla ya Usiku wa Kizimkazi tarehe 13 Agosti 2026, Mkoa wa Kusini Unguja. Aidha, anatarajiwa kushiriki kilele cha Tamasha hilo tarehe 14 Agosti 2026, kitakachofanyika katika Uwanja wa Mwehe, Kizimkazi

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii