Trump aagiza mapitio ya ratiba ya chanjo za Watoto

Rais wa Marekani, Donald Trump ametia saini agizo la kiutendaji kufikiriwa upya kwa sheria zinazolazimisha watoto wa shule kupewa chanjo za lazima, akirejelea wito wa kutaka chanjo ya surua, matumbwitumbwi na rubella igawanywe katika dozi tatu tofauti.

Hatua hiyo imekosolewa vikali na wataalamu wa afya wanaosema haina msingi wa kisayansi na inaweza kuhatarisha afya ya umma.

Aidha amri hiyo inazishauri majimbo na maeneo ya Marekani kupitia upya masharti ya chanjo kwa watoto wanaoandikishwa au kuhudhuria shule.

Udhibiti wa chanjo umekuwa moja ya ajenda kuu ya waziri wa afya wa Marekani, Robert F Kennedy, ambaye alianzisha taasisi isiyo ya kiserikali kupinga utoaji wa chanjo akijaribu kudai kuwa kuna uhusiano kati ya chanjo hizo na usonji kwa watoto.

Trump pia ameagiza wizara ya afya na uduma za kibinadamu kuunda kikosi kazi kitakachoshirikiana na sekta binafsi na mataifa mengine katika kuchunguza uwezekano wa kutoa chanjo hizo  kama chanjo tatu tofauti.

Madaktari na mashirika ya afya, hata hivyo, wanasema kuna ushahidi wa miongo kadhaa unaothibitisha usalama na ufanisi wa chanjo hizo, huku Rais wa Chama cha Madaktari wa Watoto Marekani, Andrew Racine, akisema kuwa  inaweza kuchukua zaidi ya muongo mmoja kutengeneza na kuidhinisha chanjo hizo zikiwa zimetenganishwa.

Seneta Bill Cassidy, ambaye ni daktari, pia amepinga hatua hiyo, akisema inaweza kuongeza kusita kwa wazazi kuwapeleka watoto kupata chanjo na hivyo kuwaweka watoto katika hatari zaidi.

Hatua hiyo ya Trump inakuja wakati Marekani ikikabiliwa na mlipuko mkubwa zaidi wa surua katika takriban miaka 35, huku watoto wengi wakijiandaa kurejea shuleni.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii