Kocha wa Gusa, Achia, Twende kwao Ramovic Atajwa Kutua Yanga

Klabu ya Yanga  inaelezwa kuwa katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kumrejesha aliyekuwa kocha wake mkuu, Sead Ramovic, raia wa Ujerumani, ili kukinoa kikosi hicho katika kipindi hiki cha msimu wa 2026/27.

Ramovic anatajwa kuwa miongoni mwa makocha wanaopewa nafasi ya kurejea Jangwani baada ya uongozi wa klabu hiyo kuachana na kocha Manqoba Mngqithi Oktoba 24, 2026, kufuatia matokeo yasiyoridhisha katika baadhi ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na baadhi ya vyombo vya habari vya michezo, mazungumzo kuhusu kurejea kwa Ramovic yameendelea, huku taarifa nyingine zikidai kuwa makubaliano ya awali yamefikiwa na kinachosubiriwa ni kukamilisha taratibu za mwisho.

Kocha huyo anatarajiwa kuwasili nchini leo Oktoba 30, 2026, kwa ajili ya hatua zinazohusiana na uwezekano wa kurejea kuitumikia klabu hiyo.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna uthibitisho rasmi wa Yanga kuhusu kukamilika kwa dili hilo au kusainiwa kwa mkataba mpya.

Kurejea kwa Ramovic kutakuwa habari kubwa kwa mashabiki wa Wananchi, hasa kutokana na kumbukumbu alizoacha katika kipindi chake cha kwanza Jangwani, ambacho kilikuwa kifupi lakini kilivutia kutokana na namna alivyotaka timu yake icheze soka la kasi, presha na mashambulizi ya haraka.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii