Spika wa Bunge la Kitaifa la Kenya, Moses Wetang’ula, amefichua tukio la mbunge mmoja kunaswa na kamera za usalama za Bunge (CCTV) akichukua simu ya mkononi ya mwenzake na kuiweka mfukoni, kabla ya kukana kitendo hicho hata baada ya kuoneshwa video iliyorekodi tukio hilo.
Wetang’ula amesema tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022, wakati Bunge lilipokuwa katika mvutano wa kisiasa uliotokana na mgawanyiko wa wabunge kuhusu upande uliokuwa na wingi wa idadi ya wajumbe.
Akisimulia tukio hilo, amesema alikagua picha za CCTV akiwa pamoja na Kiongozi wa Wengi Bungeni, Kimani Ichung’wah, pamoja na wabunge wengine wawili, ambapo walimshuhudia mbunge huyo akichukua simu ya mwenzake na kuiweka mfukoni.
Amesema baada ya kubaini tukio hilo, mbunge huyo aliitwa na kuulizwa kuhusu kitendo hicho, lakini alikana kuhusika licha ya kuoneshwa video iliyokuwa ikionesha wazi tukio lenyewe.
Wetang’ula alieleza tukio hilo Jumanne jioni, Novemba 24, 2026, alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Embakasi Magharibi, Mark Mwenje, aliyeomba kamera za CCTV zikaguliwe ili kuondoa tuhuma zilizokuwa zikimhusisha na kucheza michezo ya video kwenye simu wakati Bunge likiendelea na shughuli zake.
Mwenje alikuwa ameomba uchunguzi huo baada ya jina lake kuhusishwa na madai ya mbunge mmoja kucheza michezo ya video ndani ya Bunge takribani wiki mbili au tatu zilizopita.
Alisema madai hayo yalisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kufikia hata familia yake, akieleza kuwa watoto wake walianza kumuuliza kuhusu tuhuma hizo zilizokuwa zikimhusisha.
Akijibu ombi hilo, Wetang’ula alisema anaamini Mwenje hakuhusika na tukio hilo, akimtaja kuwa mbunge anayetekeleza majukumu yake ya uwakilishi, utungaji sheria na usimamizi wa shughuli za Serikali kwa uwajibikaji.
Aidha, Spika huyo aliwataka wabunge kuzingatia maadili ya uongozi na nidhamu ndani ya Bunge, akisisitiza umuhimu wa kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria.
Kauli ya Wetang’ula imeibua mjadala kuhusu nidhamu, uaminifu na uwajibikaji wa wabunge ndani ya Bunge la Kenya, huku akitumia tukio hilo kusisitiza umuhimu wa viongozi kuwa mfano wa kuigwa katika utendaji wao wa kila siku.