Wafungwa Watoroka Jela Msumbiji Kisa Uchaguzi

Zaidi ya wafungwa 1, 500 wametoroka katika gereza moja nchini Msumbiji, wakitumia fursa ya machafuko ya kisiasa yanayoendelea yaliyochochewa na matokeo ya uchaguzi wenye utata, polisi wamesema.

Watu 33 waliuawa na 15 kujeruhiwa katika mapigano na walinzi, mkuu wa polisi Bernardino Rafael aliambia mkutano na waandishi wa habari. Takriban watoro 150 zaidi wamekamatwa tena, aliongeza.

Maandamano yalizuka siku ya Jumatatu kujibu mahakama ya juu zaidi ya Msumbiji iliyothibitisha kwamba chama tawala cha Frelimo, kilichokuwa madarakani tangu mwaka 1975, kilishinda uchaguzi wa rais wa Oktoba.

Bw Rafael alisema makundi ya waandamanaji wanaoipinga serikali yalikaribia gereza hilo katika mji mkuu Maputo siku ya Jumatano. Wafungwa walitumia machafuko hayo kuangusha ukuta na kutoroka, alisema.

Msumbiji imekumbwa na machafuko tangu uchaguzi uliozozaniwa mwezi Oktoba. Matokeo rasmi yalionyesha mgombea urais wa chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo, akishinda huku wapinzani wakipinga na kusema wameiba kura.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii