Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania wenye uwezo wa kifedha kuwekeza ndani ya nchi, akisisitiza kuwa njia hiyo ndiyo mwarobaini wa kupunguza ukosefu wa ajira na kukuza uchumi wa Taifa.
Akizungumza hayo Juni 16, 2025 mkoani Simiyu muda mfupi baada ya kuzindua kiwanda cha mabomba na kuchakata pamba Rais Samia amesema kuwa sekta ya viwanda ina mchango mkubwa katika maendeleo hivyo Watanzania hawapaswi kusubiri misaada au mikopo kutoka nje.
Aidha ameeleza kuwa wanataka pamba itengenezwe hapa hapa ili wananchi wa Simiyu wapate ajira ndani ya mkoa huu vilevile Watanzania ambao wamejaliwa vijisenti, waweze kuwekeze ndani ili kutengeneza ajira na kukuza uchumi wa nchi yetu wenyewe, badala ya kutegemea mikopo na misaada kutoka nje ya nchi.
Ziara hiyo ya Rais Samia mkoani Simiyu inahusisha uzinduzi wa miradi sita ya kimkakati ambayo inalenga kuimarisha uchumi wa wananchi na kuleta maendeleo ya haraka.