Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu ambayo imeguswa na mzozo mkubwa wa ukwasi unaohusishwa kwa kiasi kikubwa na kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani, imelazimika kutangaza wiki iliyopita kusimamishwa kwa ujumbe wa kutafuta ukweli wa kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu uliofanyika mashariki mwa DRC tangu mwezi Januari 2022.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu. Taasisi hiyo ambayo imeguswa na mzozo mkubwa wa ukwasi, imelazimika kutangaza kusitishwa kwa ujumbe wa uchunguzi wa uhalifu uliofanyika mashariki mwa DRC. Ujumbe huo ulikuwa umeanza kazi kwa ufadhili wa dola milioni 1.1 kutoka kwa akiba yake ya dharura. Juhudi zake tayari zilifanya ukusanyaji wa "kiasi kikubwa cha ushahidi kutoka kwa wahasiriwa na mashahidi nchini DRC, Rwanda, na Burundi, pamoja na nchi zingine," kulingana na Volker Türk, mkuu wa ofisi hiyo.
Mchakato uliokuwa na lengo la "kukusanya, na kuchambua ushahidi" wa madai na ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa tangu Januari 2022 katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini ulizinduliwa mwezi Februari mwaka jana kufuatia kupitishwa kwa azimio la Baraza la Haki za Kibinadamu linalotaka kuanzishwa kwa haraka kwa ujumbe wa kutafuta ukweli na tume ya uchunguzi iliyoundwa na wataalam watatu huru.
Katika barua ya ndani iliyoonekana na wenzetu kutoka sirika la habari la REUTERS, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Türk, alitangaza wiki iliyopita kwamba tume hii haiwezi kuanzishwa "mpaka fedha zipatikane." "Hali inatia wasiwasi sana," amebainisha mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC. Katika barua pepe kwa RFI, Kamishna Mkuu anasikitika kwamba hatua zinazofuata katika mchakato huo haziwezi kukamilika "kwa kuzingatia kushuka kwa dola milioni 60 kwa michango ya hiari ikilinganishwa na mwaka 2024," kabla ya kutoa maoni haya ya uchungu: "Hatuko katika nafasi ya kuanza kazi ya tume ya uchunguzi kama ilivyopangwa."
Sababu hasa ni kusitishwa kwa baadhi ya michango—hasa kutoka Marekani—miezi michache iliyopita. Wakati Washington ilikuwa bado mfadhili mkuu wa taasisi hiyo mwaka jana, ikiwa na mchango wa dola milioni 36, mchango wake katika ufadhili wake ulishuka hadi sifuri kufikia Mei 31.
Wakati Volker Türk alionya siku chache zilizopita kwamba "kupunguzwa kwa ufadhili kwa ofisi [yake] [...] kunaimarisha tu nafasi ya madikteta na viongozi wa kimabavu," wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa hawakati tamaa: katika barua pepe kwa RFI, wanahakikisha kwamba uchunguzi nchini DRC utaanza tena punde tu fedha zitakapotolewa kwao.