Kikosi cha wanajeshi kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kimewasili nchini Comoro, ambapo kinatarajiwa kushiriki maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa nchi hiyo yatakayohudhuriwa pia na Rais Samia Suluhu Hassan atakayekuwa mgeni rasmi.
Kikosi hicho kikiongozwa na Kapteni Mohammed Nchimba kimetembelea ubalozi wa Tanzania nchini Comoro na kukutana na Balozi Saidi Yakubu pamoja na Mwambata Jeshi, Kanali Abdulrahim Mahmoud Abdallah ambaye anaratibu ziara hiyo.
Akizungumza na askari hao Balozi Yakubu ameushukuru uongozi wa JWTZ hususan Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Nkunda kwa kukubali mwaliko wa Jeshi la Comoro na kutuma kikosi chake kunogesha maadhimisho hayo. Mbali na Tanzania, wanajeshi kutoka China na Morocco nao pia watashiriki.
Balozi Yakubu pia amesema kuwa ushiriki wa JWTZ katika maadhimisho hayo ni kielelezo cha ushirikiano wa majeshi ya nchi hizo mbili na kuwaeleza kuwa vikosi vya JWTZ wamekuwa ni kivutio kikubwa wanaposhiriki na hivyo mwaka huu ni matarajio ya Wacomoro kuwa hali hiyo itaendelea na kuwaeleza pia makundi mengine yanayoshiriki kutoka Tanzania yallyoalikwa ikiwemo vikundi vya burudani na mabondia.