Serikali imesema imekuwa ikiongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu mwaka hadi mwaka ili kuwawezesha wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalumu na wanaotoka kwenye familia zenye uwezo mdogo wa kiuchumi ili kuwawezesha kumudu gharama za masomo ya elimu ya juu na kufikia ndoto zao.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Dtk. Paulina Nahato aliyetaka kujua Serikali haioni haja ya kuongeza fedha za mkopo kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wenye mahitaji maalumu.
Amesema fedha za mikopo zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 464 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 787 mwaka 2024/2025, na idadi ya wanufaika imeongezeka pia kutoka wanafunzi 145,000 mwaka 2020/2021 hadi 235,799 mwaka 2024/2025 wakiwemo wenye mahitaji maalumu.
Aidha amesema kwa sasa utoaji mikopo unawapa ahueni wanafunzi wenye mahitaji maalumu au wenye wazazi wenye ulemavu kwa kuwapatia kipaumbele katika upangaji wa mikopo ili kuwawezesha kumudu mazingira ya chuo katika kipindi cha masomo yao.
Jumla ya wanafunzi 2,398 wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2024/2025 kupitia kigezo cha mahitaji maalumu ambapo Serikali imeendelea kupokea ushauri na maoni ya wadau kwa ajili ya kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na wadau ili kubainisha aina ya uhitaji unaostahili kupewa kipaumbele bila kuathiri dhana ya uhitaji inayotamkwa na sheria.