Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imebaini mbinu mpya inayotumiwa na wasafirishaji wa dawa za kulevya kwa kutumia pipi za watoto kama kificho ili kufanikisha kusafirisha dawa hizo haramu.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema hayo Juni 26, 2025 jijini Dodoma katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Matumizi na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya.
Lyimo amesema matumizi ya pipi kuficha dawa za kulevya ni njia ya kihalifu inayoashiria namna biashara hiyo imeendelea kubadilika na kuwa hatari zaidi, hasa kwa kuwalenga watoto na vijana.
Mbinu hii ni ya hatari sana kwa sababu inalenga moja kwa moja kundi la watoto. Hii ni sehemu ya jitihada kubwa tunazozifanya katika kudhibiti uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini .
Ameeleza kuwa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola itaendelea kuwa makini na kutumia teknolojia ya kisasa kubaini mbinu mpya zinazotumiwa na wahalifu wa dawa za kulevya.