Vita baridi ndani ya upinzani miongoni mwa vinara wake uchaguzi wa 2027 ukinukia

JAPO la muungano wa upinzani linaonekana kuwa na mshikamano, mvutano unatokota miongoni mwa vinara wake, hali inayoweza kuvuruga mpango wake wa kudhamini mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Vinara wa muungano huo ni pamoja na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua (ambaye ni kiongozi wa chama cha Democracy for Citizen’s Party-DCP), Kalonzo Musyoka (Wiper), Eugene Wamalwa (DAP-K), Martha Karua (PLP), Justin Muturi (DP), Torome Saitoti (mwenyekiti wa Jubilee) na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Fred Matiang’i.

Hata hivyo, Bw Gachagua, anayeonekana kama kiongozi wa mrengo huo, amepuuzilia mbali hofu kwamba kuna migawanyiko kati yao akiahidi kufaulisha azma ya kumng’oa mamlakani Rais William Ruto.

Lakini, bila ‘kutakaswa’ na mahakama, Bw Gachagua aliyeondolewa mamlakani Oktoba 8, 2024 hawezi kuwania urais wala kushikilia kiti chochote cha umma.

Mnamo Jumatano, mbunge huyo wa zamani wa Mathira, Nyeri alisema kuwa wakazi wa Mlima Kenya wako tayari kumpigia kura Mkenya mwingine ili awe rais baada ya kusalitiwa na Dkt Ruto waliyempigia kura kwa wingi mnamo 2022.

Hata hivyo, wanasiasa wa upinzani wameidokezea Taifa Leo kwa mvutano wa kimamlaka tayari unatokota miongozi mwa vinara wa upinzani.

Kwa mfano, chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyataa na DCP cha Bw Gachagua, tayari vimeanza kuvutana kuhusu mpeperushaji bendera ya urais wa upinzani.

Jubilee inamtaka Dkt Matiang’i hali DCP inamuunga Bw Musyoka ambaye ni kiongozi wa Wiper. Jubilee, kupitia katibu mkuu, Bw Jeremiah Kioni inamtaka Dkt Matiang’i kama “mwanamageuzi mwenye tajriba na aliye na sifa hitajika za kuongoza taifa hili”.

Lakini katika mahojiano ya majuzi katika runinga moja ya humu nchini, waziri huyo wa zamani wa Usalama alijitenga na dhana kwamba yeye ni mradi wa Bw Kenyatta.

Alisisitiza kuwa lengo lake ni kusaka ufuasi kote nchini ili aweze kuwahudumia Wakenya wote kwa usawa.

Hatua ya Jubilee kuunga Dkt Matiang’i imewakasirisha wafuasi wa chama cha DCP chenye ufuasi mkubwa katika eneo la Mlima Kenya.

Aidha, Gachagua mwenyewe alimshauri Matiang’i kubuni chama chake cha kisiasa huku akimwonya dhidi ya kutegemea uungwaji wa Jubilee.

Eneo la Magharibi, mvutano mwingine unatokota kati ya kiongozi wa DAP-K, Bw Wamalwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya.

Japo Bw Natembeya ni ‘mtoto’ kisiasa kwa Bw Wamalwa kwani alitumia chama chake kuwania ugavana 2022, Gavana huyo amevutia ufuasi sana.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii