Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Marco Rubio amehitimisha siku yake ya pili na ya mwisho kwenye mkutano wa usalama wa Jukwaa la Kikanda la Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN nchini Malaysia.
Rubio amefanya mkutano na waziri mwenzake wa China Wang Yi huku mvutano ukiongezeka kati ya Washington na Beijing kuhusu masuala kuanzia biashara hadi usalama na uungaji mkono wa China kwa vita vya Urusi nchini Ukraine. Rubio na Yi hawakuzungumza na waandishi habari baada ya mazungumzo yao ya ana kwa kwa ana.
Mkutano wao ulifanyika chini ya saa 24 baada ya Rubio kukutana mjini Kuala Lumpur na mpinzani mwingine, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov, ambapo walijadili njia mpya za kuanzisha mazungumzo ya amani nchini Ukraine.
Mikutano hiyo inajiri wakati kukiwa na wasiwasi wa kimataifa na wa kikanda kuhusu sera za Marekani, hasa juu ya biashara na ushuru mkubwa ambao Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuwatoza washirika wake na hata na maadui zake.