Idadi ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo mkali katika jimbo linalokumbwa na vita la Darfur Kaskazini imeongezeka maradufu tangu mwaka jana, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) limetangaza leo Ijumaa.
Tangu mwezi Aprili 2023, vita kati ya jeshi la Sudani na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vimeua makumi ya maelfu ya watu na kuwalazimu zaidi ya milioni 14 kukimbia makazi yao.
Jimbo la Darfur Kaskazini na mji mkuu wake uliozingirwa, El Fasher, yameathirika sana, huku njaa ikitangazwa mwaka jana katika kambi tatu kubwa za watu waliokimbia makazi yao nje ya mji huo.
Katika taarifa iliyotolewa leo Ijumaa, UNICEF imeripoti kuwa zaidi ya watoto 40,000 wanaokabiliwa na utapiamlo mkali huko Darfur Kaskazini walilazwa kwa matibabu kati ya mwezi wa Januari na Mei mwaka huu, mara mbili zaidi ya kipindi kama hicho mwaka jana.
"Watoto huko Darfur wana njaa kutokana na migogoro na kunyimwa misaada ya kuokoa maisha," amesema Sheldon Yett, Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudani.
Katika majimbo matano ya Darfur, visa vya utapiamlo mkali viliongezeka kwa asilimia 46 katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.
Vita vya El Fasher—jiji kuu la mwisho huko Darfur ambalo bado liko chini ya udhibiti wa jeshi— vimezidi katika miezi ya hivi karibuni.
Hospitali zimeshambuliwa kwa mabomu, misafara ya misaada ya kibinadamu imeshambuliwa, na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu sasa umezuiwa kabisa.
Umoja wa Mataifa uliripoti wiki hii kwamba karibu 40% ya watoto chini ya miaka mitano huko El Fasher wanakabiliwa na utapiamlo mkali, ikiwa ni pamoja na 11% wakikabiliwa na utapiamlo mkali sugu.
UNICEF pia imeripoti ongezeko kubwa la utapiamlo katika maeneo ya vita hivi karibuni.
Utapiamlo mkali umeongezeka kwa zaidi ya 70% katika Jimbo jirani la Kordofan Kaskazini, kwa 174% katika mji mkuu Khartoum, na karibu mara saba katika jimbo la kati la Al Jazeera.
Khartoum na Al Jazeera zilitekwa tena na jeshi mapema mwaka huu, lakini nchi hiyo bado imegawanyika.
Jeshi linadhibiti mashariki, kaskazini na katikati, wakati RSF inadhibiti karibu Darfur yote na sehemu za kusini.