MBUNGE wa Naivasha, Jayne Kihara, ameagizwa kufika mbele ya wapelelezi katika Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Jumba la Mazingira, Barabara ya Kiambu, Nairobi, leo kuhusiana na madai kuwa alichochea chuki.
Kulingana na agizo hilo, Mbunge alitoa kauli ambazo zinaweza kuwafanya raia kuwachukia maafisa wenye mamlaka serikalini.
“Kitengo cha uchunguzi katika DCI kilichoko katika makao makuu kinachunguza madai ya kosa la kuhujumu mamlaka ya afisa wa umma kinyume na sehemu 132 ya Sheria ya Uhalifu, Sura ya 63 ya Sheria za Kenya baada ya malalamishi kuhusu usambazaji wa kauli za uchochezi kuwasilishwa,” ikasema hati ya agizo hilo iliyotiwa saini na Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchunguzi, George Lenny Kisaka.
Kwa hivyo, afisa huyo anamtaka Mbunge huyo kufika mbele yake afisini mwake katika makao makuu ya DCI leo Julai 14 mwaka huu saa nne na nusu asubuhi, kudadisiwa kuhusiana na suala hilo la madai ya kutoa matamshi ya chuki.
Lakini Mbunge huyo alikuwa mwepesi kudai kuwa DCI inamwandama kutokana na kauli kali ambazo amekuwa akitoa akiilaumu serikali kuhusiana na mwenendo wa polisi kuwaua raia kiholela nyakati za maandamano katika siku za hivi karibuni.
“Nadhani ni kuhusiana na hutoba yangu wakati wa mazishi ya Boniface Kariuki katika Kaunti ya Murang’a mnamo Ijumaa ambapo nilisema wazi kwamba serikali ndiyo ya kulaumiwa kwa kifo cha kijana huyo,” akasema Bi Kihara, ambaye ni mwandani wa aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua.
Marehemu Kariuki, ambaye alikuwa muuzaji wa barakoa, alipigwa risasi na polisi katikati mwa jiji la Nairobi mnamo Juni 17, wakati wa maandamano ya kulaani mauaji ya mwanablogu Albert Ojwang’.
Alikufa mnamo Juni 30, siku 13 baada ya kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) na akazikwa mnamo Julai 11 mwaka huu nyumbani kwao katika eneobunge la Kangema, Kaunti ya Murang’a