Juba inajaribu kuimarisha tena uhusiano wake na Washington

Nchini Sudan Kusini nyaraka za siri zilizovuja kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha kuwa, serikali jijini Juba imekuwa ikijaribu kuimarisha tena uhusiano wake na Marekani ambao umeendelea kuyumba katika miaka ya hivi karibuni.

Nyaraka hizo ambazo zimethibitishwa kuwa za kweli na hata kuchapishwa kwenye tovuti ya Wizara inayoshughulikia masuala ya sheria nchini Marekani, zimebaini kuwepo kwa mkataba wa maelewano kati ya serikali ya Sudan Kusini na kampuni moja ya Marekani, ili kuisaidia kuimarisha uhusiano na Washington.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo serikali ya Juba, imeilipa kampuni hiyo Scribe Strategies & Advisors Dola Laki tano, ili kuisaidia katika kurejesha tena uhusiano na Marekani.

Licha ya nyaraka hizo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kwa siku tatu, serikali ya Juba, imeendelea kusalia kimya, huku ikibainika kuwa Balozi wa Sudan Kusini jijini Washington, Aprili 25, aliiandikia barua kampuni hiyo, kuomba msaada.

Viongozi wa mashirika ya kiraia nchini Sudan Kusini, wakiongozwa na Edmund Yakani wanataka serikali ya Juba kuzungumzia taarifa hizo kwa uwazi, huku ikielezwa kuwa ili kurejesha uhusiano, Juba iko tayari kuwapokea wahamiaji kutoka Marekani ambayo imewawekea baadhi ya maafisa wake vikwazo kutokana na vita vya mara kwa vita vinavyoendelea.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii