Mazungumzo ya amani yakwama mjini Doha, Qatar

Rais wa Marekani kwa mara nyingine anajifanya msuluhishi na mtetezi wa amani, huku mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja mjini Doha, Qatar, yaliyoanza Julai 6, yakionekana kukwama katika siku za hivi karibuni. Nchini Israeli, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu bado anajaribu kushawishi mrengo wa kulia wa muungano wake kukubali kusitishwa kwa mapigano

Jaribio la kuanzisha tena mazungumzo juu ya usitishaji vita huko Gaza huku uhai wa muungano wa serikali ya Israel ukitakiwa kuzingatiwa, kwa hakika, ulikuwa lengo kuu la mjadala wa baraza la usalama la Israeli. Hii ni pamoja na suala la kutumwa tena kwa wanajeshi wa Israeli, anakumbuka mwandishi wetu huko Jerusalem, Michel Paul.

Kama tunavyojua, mazungumzo yanakwama hasa juu ya suala la Morag Corridor. Huu ni mstari wa kuvuka kusini mwa Ukanda wa Gaza, kati ya miji ya Rafah na Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, ambapo Israeli inataka kudumisha ngome zake kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya kuwakusanya tena idadi kubwa ya wakazi wa Gaza katika eneo hili. Hamas inapinga hili kwa kiasi kikubwa.

Israel inatazamiwa kutuma mpango mpya kwa wapatanishi katika mji mkuu wa Qatar kwa mara nyingine tena leo , Julai 14. Mrengo wa kulia wa serikali ya Israeli, hususan mawaziri wenye msimamo mkali Ben Gvir na Smotrich, wanadai kuhakikishiwa kwamba vita vya Gaza vinaweza kuanza tena baada ya kusitisha mapigano kwa siku 60. Na wanatishia kujiuzulu.

Mbele ya ofisi ya Waziri Mkuu, familia zilizokata tamaa za mateka zilijitokeza wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri. Rasmi, mazungumzo huko Doha yanaendelea, lakini kwa matumaini madogo sana katika hatua hii.

Makumi ya watu waliuawa huko Gaza kwa siku moja

Katika eneo lililozingirwa, Wapalestina 43 waliuawa iku ya Jumapili na mashambulizi ya anga ya Israeli, msemaji wa shirika la Ulinzi wa Raia Mahmoud Bassal amesema. Miongoni mwao, Wapalestina 11, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, waliuawa katika shambulio kwenye soko katika mji wa Gaza, kaskazini mwa eneo hilo, na wengine watatu katika kambi ya wahamiaji ya Al-Mawassi kusini.

Katika mji wa Nuseirat, katikati mwa Gaza, watu 20 waliuawa, kumi kati yao ikiwa ni pamoja na watoto karibu na kituo cha kusambaza maji ya kunywa, msemaji wa shirika la Ulinzi wa Raia ameongeza.

Jeshi la Israeli lilisema lilimlenga mwanachama wa Islamic Jihad, kundi lenye silaha linaloshirikiana na Hamas, lakini likakiri kwamba "mabomu hayo yalianguka umbali wa mita kadhaa kutoka kwake" kutokana na "makosa ya kiufundi." "Tukio hilo linachunguzwa," jeshi limeongeza.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii