Wakati wajumbe kutoka serikali ya Kongo na vuguvugu la waasi la AFC/M23 wanakutana mjini Doha kujaribu kuelekea kwenye makubaliano ya amani, mivutano inaendelea. Katika mazingira haya ya mvutano, wapatanishi wanafanya kazi kwa bidii.
Kinshasa inaripoti harakati za mara kwa mara za askari na vifaa kutoka kwa AFC/M23 na washirika wake kwenye mstari wa mbele. Katika Baraza la Mawaziri la mwishoni mwa juma lililopita, serikali ilitoa tahadhari: Idadi kubwa ya vikosi vya waasi imeonekana katika mkoa wa Kivu Kusini. Lengo, kulingana na Kinshasa, ni kuteka maeneo mapya, hasa jiji la kimkakati la Uvira, ambalo bado liko chini ya udhibiti wa FARDC.
Katika mazingira haya ya wasiwasi, wapatanishi wanatumai kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo. Mamlaka ya Qatar inataka kuchukua hatua haraka. Wanatumai kuona makubaliano ya amani yakihitimishwa wiki hii mjini Doha kati ya serikali ya Kongo na AFC/M23.
Ni katika muktadha huu ambapo wawezeshaji wa Kimarekani nao wamefika mjini Doha. Alipoulizwa na RFI kuhusu jukumu lao, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amethibitisha kuwepo kwa Marekani kama waangalizi: "Tunaendelea kuratibu kwa karibu na Qatar na washirika wengine ili kuhakikisha kwamba juhudi zote zinakutana kuelekea lengo moja la amani ya kudumu."
Kulingana na RFI, majadiliano kwa sasa yanalenga tamko la kanuni, sharti la makubaliano ya mwisho. Lengo ni kukamilisha nakala zote mbili mwishoni mwa juma.
Kuhusiana na ombi la AFC/M23 la kuachiliwa kwa wafungwa wake, chanzo cha Kongo kilmeiambia RFI kwamba hili litafanywa kwa msingi wa kesi baada ya kesi, na sio kwa jumla.
Kwa upande wa Kongo, wajumbe hao wanaongozwa na Sumbu Sita Mambu, Mwakilishi Mkuu wa Mkuu wa Nchi. Kwa upande mwingine, AFC/M23 inawakilishwa na Benjamin Bonimpa, katibu mkuu wa vuguvugu hilo.
Kulingana na RFI, Mawaziri wa Mambo ya Ndani wa Rwanda, Vincent Biruta—aliyepo Doha kama mwangalizi—na wa DRC, Jacquemain Shabani, pia walizungumza. Mazungumzo yao yaklifanyika kwa siri na yalilenga kufafanua majukumu yao katika kuunga mkono mchakato huo, kwa mujibu wa makubaliano yaliyotiwa saini mjini Washington tarehe 27 Juni.