WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza usimamizi wa ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara ikiwemo wa mataifa ya nje walioamua kuja kufanya shughuli zao nchini.
Amesema kuwa TRA inapaswa kuongeza ufanisi zaidi kwenye kuwasimamia wafanyabiashara wote kuhakikisha wanatambua sheria za ulipaji kodi pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakiki utekelezaji wake.
Ametoa agizo hilo leo Julai 08 huu alipofungua kikao kazi cha Viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kituo cha Mikutano cha Arusha (IACC).
“Nendeni mkachunguze hawa wanaokuja kufanya biashara nchini, kama wanaondoka na mapato yetu kwa kutolipa kodi yetu, ni lazima tubane eneo hilo kama ambavyo sisi tunabanwa tunapokwenda kwao, yeyote aliyeamua kuja kufanya biashara Tanzania ni lazima ajue Tanzania ina sheria zake ikiwemo za ulipaji kodi”
Aidha Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza TRA kwa kufanikiwa kukusanya Shilingi Trilioni 32.26, sawa na ufanisi wa asilimia 103.9 dhidi ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 31.05.
“Hii ni hatua ya kihistoria na ya kujivunia kwa kuwa ni mafanikio yanayoakisi dhamira, weledi, na juhudi mlizonazo zinazofanywa na timu ya TRA na uongozi wote katika kuhakikisha mnafikia malengo mliojiwekea”
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Fedha kuendelea kufanya maboresho ya Sera sheria na kuimarisha mifumo ya kodi ili kufikia wigo wa juu wa ukusanyaji kodi bila kuathiri ustawi wa shughuli za kiuchumi.