Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimetangaza kuanza awamu ya pili ya ziara yake katika maeneo mbalimbali ambayo kimeiita ziara hiyo kuwa CHAUMMA For Change phase 2 (C4C2) 9 Julai 2025 ambapo ziara hiyo itaendelea kwa siku kadhaa mbele.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam Jumanne Julai 8 mwaka huu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Habari na Taarifa kwa Umma wa CHAUMMA, John Mrema, amesema kuwa kwa siku hiyo ziara itaanzia kisiwani Pemba katika Uwanja wa Gombani huku kwa siku ya Alhamisi itakuwa zamu ya Unguja.
Ameeleza kuwa ziara hiyo itaongozwa na viongozi wakuu wa chama wakiambatana na Mwenyekiti wetu Hashim Rungwe, tarehe 11 tutakwenda Tanga kumalizia kiporo ambacho tulikiacha baada ya ratiba yetu kugongana na ratiba ya Mwenge.
Aidha Chama cha Ukombo (CHAUMMA) kimesema maandalizi ya ilani yake ya uchaguzi kwa mwaka 2025 yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 95, huku ikitaja kuwa mwelekeo wa ilani hiyo ni kuwa ya wananchi kwa wananchi.
Hata hivyo John Mrema amesema kuwa chama hicho kimeweka mbele maslahi ya wananchi kwa kujenga hoja, kutambua changamoto na kupendekeza suluhisho lenye mwelekeo wa kuleta maendeleo jujumuishi.
Na amebainisha kuwa mnamo Julai 7, mwaka huu viongozi wakuu wa chama hicho walipokea rasmi Rasimu Sifuri ya Ilani, hatua ambayo inafungua mlango wa kuanza kwa vikao vya ndani na majadiliano ya mwisho kabla ya kuzinduliwa rasmi kwa ilani hiyo ya uchaguzi.
Hivyo Kwa mujibu wa Mrema CHAUMMA itahakikisha ilani hiyo inaakisi hali halisi ya jamii ya Kitanzania na kuwa nyenzo ya mabadiliko ya kweli.