Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya DCEA imeeleza kubaini na kuwakamata wamiliki wa kiwanda bubu cha kuzalisha biskuti zenye viambata vya dawa za kulevya aina ya bangi na skanka eneo la Sinza jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na vyombo vya habari Julai 09, 2025 Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema kiwanda hicho wamekibaini jana Julai, 08, 2025 majira ya mchana na walifanikiwa kuwakamata wamiliki na kuwadhibiti.
“Eneo la Sinza walikamatwa watu wawili wamiliki wa kiwanda bubu kinachotengeneza biskuti zinazochanganywa na bangi kisha kuzisambaza katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Lindi na Mtwara.”
Ameeleza kuwa wazalishaji wamekuwa wakiwauzia zaidi wafanyabiashara wa madini lengo likionekana ni kwenda kuwapa wale wanaofanya nao biashara hizo ili wakilewa waweze kuwaibia.
“Wakati huohuo mkoani Lindi alikamatwa mfanyabiashara wa madini akisambaza biskuti zilizochanganywa na bangi”
Lyimo ameeeleza kuwa mfanyabiashara huyo mkubwa wa madini wa mkoani Lindi walimkuta akiwa na biskuti hizo na tayari wamemshikilia kwa ajili ya kumchukulia hatua zaidi za kisheria, huku akitoa onyo kwa yeyote atakayejihusisha na biashara hiyo kuwa hatofanikiwa.