Prof.Kabudi "Kuna mambo yanaonekana ya kipuuzi ila kwa nchi yetu ni muhimu"

Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzania ndio nchi pekee ni Taifa, na kwamba nchi nyingine za Afrika ni mkusanyiko wa makabila.

Akiwasilisha mada ya uzalendo leo Julai 9,2025 wakati wa mkutano wa wadau kujadili mchango wa sekta ya habari katika kufanikisha Uchaguzi Mkuu 2025,amesema kama Taifa tuna mambo yetu tunayoyaamini lazima yaheshimiwe.

"Wengi hawafahamu kama sisi ni Taifa lenye utofauti wa makabila na lugha nyingi.Sisi ndio taifa kubwa lenye utofauti wa mila,tamaduni na desturi na tunaishi kwa umoja na upendo. Leo hii huwezi kusema chakula hiki ni chakula cha Taifa,"amesema Prof.Kabudi.

Aidha,amesema kwasasa serikali imeanzisha utaratibu wa kuiandikisha Tanzania kama Taifa lenye lugha nyingi.

"Tusipoelewa hili tutaanza kuiga waliopo kwenye mkusanyiko wa makabila,tusipokuwa makini tutaendelea kuwaabudu wenye mkusanyiko."

Amesema Taifa la Tanzania ni matokeo ya hiyari ya kuungana na Tanganyika na Zanzibar, lenye makabila zaidi ya 160 na ndani ya kabila moja kuna makabila mengi.

Amesema Taifa na Umoja vinapaswa kulindwa kwa wivu mkubwa,na kwamba mataifa yote yanayojitambua na kujithamini yanavitu ambavyo wengine wanaviona vya kipuuzi lakini ni vya maana na ni alama ya kuwatambulisha.

"Tuna vitu watu wataona ni vya kupuuzi pamoja na majirani, ila kwetu ni vya msingi sana Mfano Mwenge wa Uhuru,tukianza kuvidharau tunavunja umoja wetu na utaifa wetu.

"Moja ya jambo linaloonekana ni ujinga ni Mwenge wa Uhuru Taifa,lakini ni muhimu sana kwa Tanzania na muhimu snaa kwetu, lazima liwe na ujinga ambao linaoheshimu,ambapo ujinga huo unaifanya Tanzania kuendelea kuwa Taifa."

"Kiingereza kimewafanya wengine kuwa mkusanyiko wa makabila ila Kswahili kimeifanya Tanzania kuwa Taifa moja,huko kuonekana hatumudu Kiingereza ni jambo ambalo si kweli ni jambo baya kwao ila sisi tunajivunia Kiswahili kilichotuunganisha,"amesema Kabudi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii