Jeshi la Mali na kundi la mamluki wa Urusi, Wagner, waliwaua makumi ya watu wa kabila la Fulani mwanzoni mwa mwaka huu wakati wa operesheni dhidi ya wanajihadi kaskazini mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa taarifa kutoka shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch.
Shirika hilo limesema kuwa jamii ya Fulani ambayo kwa kawaida inajulikana kwa wafugaji wa kuhamahama, wamekuwa wakibaguliwa katika eneo lote la sahel huku wakishutumiwa kushirikiana na vikundi vya Kiislamu vyenye silaha pamoja na kutoa wapiganaji vijana.
Kwenye ripoti yake, Human Rights Watch inasema, Jeshi la Mali na kundi la Wagner "huenda waliwaua takriban watu 12 toka jamii ya Fulani na wengine zaidi ya 80 wametoweka tangu mwezi Januari mwaka huu.
Machi 30, wanajeshi wa Mali na wapiganaji wa Wagner waliingia huko Belidanedji katika eneo la kati la Segou na kuwaua mamia ya raia toka jamii ya Fulani waliokuwa wakikimbia mapigano, ilisema taarifa ya shirika hilo.
Shirika hilo sasa linautaka Umoja wa Afrika kuishinikiza serikali ya Mali kufanya uchunguzi na kuwafungulia mashtaka waliohusika.