Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) mkoani Katavi kimewatoa wasiwasi wananchi wa Kata ya Kakese, Manispaa ya Mpanda, kuhusu usalama wa kura zao kwenye uchaguzi mkuu ujao, kikiahidi kuwa na mikakati madhubuti ya kuzilinda ingawa hakijaweka wazi mbinu hizo kwa sasa.
Kauli hiyo imetolewa siku ya Jumatano na Mwenyekiti wa CHAUMMA Mkoa wa Katavi, Almas Ntije, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kakese, ambapo wananchi walitaka kujua kwa kina namna chama hicho kitapambana na wizi wa kura ambao umekuwa ukilalamikiwa na vyama mbalimbali vya siasa.
Mathias Kashinje, mmoja wa wananchi waliohoji, alisema: "Tumekuwa tunapiga kura lakini mnasema zikiibiwa mtamuachia Mungu. Je, tunampigia Mungu au tunachagua viongozi? Sisi wananchi tufanyeje kulinda kura zetu?"
Akijibu, Almas Ntije alisema: “Hatutatoa wazi mikakati yetu ya kulinda kura kwa sababu hiyo ni siri ya chama, lakini tunawaomba wananchi watuamini – tutazilinda kura.”
Kwa upande wake, Kamishna wa CHAUMMA Kanda Maalum ya Magharibi, Masanja Mussa Katambi, ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, alisisitiza kuwa wizi wa kura si sababu ya kukata tamaa bali ni sababu ya kuendeleza mapambano ya kidemokrasia.
Katika mkutano huo, baadhi ya wananchi walihoji pia kuhusu hatua za chama hicho katika kushughulikia changamoto kama miundombinu mibovu ya barabara. Akijibu hoja hizo, Katambi alisema:
“Tunahitaji watu wenye uchungu wa kweli kwa wananchi. Hatutegemei miujiza, bali uwakilishi imara unaopaza sauti kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.”
Mkutano huo ulifanyika sambamba na uzinduzi wa ofisi mpya ya CHAUMMA mkoani Katavi, na ulihudhuriwa na viongozi wa ngazi ya mkoa akiwemo Mwenyekiti wa chama mkoani humo Alfonce Ntije, pamoja na wanachama waliotia nia ya kugombea nafasi mbalimbali.