Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Mashujaa yatakayofanyika Julai 25 mwaka huu katika Mnara wa Mashujaa, Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 24 mwaka huu Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema maandalizi ya tukio hilo yamekamilika, ambapo gwaride la heshima litaandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama
Dk. Biteko amesema siku hiyo ni maalum kwa ajili ya kuwakumbuka mashujaa waliotoa uhai wao, nguvu na sadaka kwa ajili ya uhuru, amani na maendeleo ya Taifa, wakiwemo waliopoteza maisha vitani na waliostaafu kwa heshima.
Aidha, amesema Mwenge wa Kumbukumbu ya Mashujaa utawashwa rasmi Julai 24 saa 6:00 usiku na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kwa niaba ya Rais, na utazimwa usiku wa Julai 25 kuashiria hitimisho la maombolezo.