Shirika la kutetea haki za binadamu duniani Amnesty International limetangaza kuwa Serikali ya Iran ilitumia mabomu ya vishada katika maeneo ya makazi wakati wa mapigano ya siku 12 kati yake na Israel, hatua ambayo imetajwa kuwa ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Katika ripoti yake mpya iliyotolewa Julai 24, Amnesty ilieleza kuwa mashambulizi hayo yalilenga maeneo yaliyo na idadi kubwa ya watu na kwa kufanya hivyo, Iran iliweka maisha ya raia wengi katika hatari kubwa.
Kwa mujibu wwa taarifa shirika hilo lilisema lilituma maswali rasmi kwa mamlaka za Iran kuhusu tuhuma hizo 15 Julai mwaka lakini hadi kufikia wakati wa kuchapishwa kwa ripoti hiyo, hakuna majibu yoyote yaliyotolewa.
Amnesty International imetumia uchambuzi wa picha na video kutoka katika eneo la Ghoshdan, nje ya mji wa Tel Aviv, ambazo ziliripotiwa kupigwa tarehe 19 Juni wakati wa mashambulizi ya Iran kwa kutumia makombora ya balestiki. Uchambuzi huo umebaini kuwepo kwa vipande vinavyoonesha matumizi ya mabomu ya vishada.
Mabomu ya vishada (cluster munitions) huachilia mabomu madogo madogo mengi ambayo hutawanyika katika eneo kubwa. Mara nyingi, mabomu haya madogo hayalipuki mara moja, na hivyo kuwa tishio la muda mrefu kwa raia – hata baada ya vita kuisha.
Kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Kupiga Marufuku Mabomu ya Vishada wa mwaka 2008, matumizi ya silaha hizo yanapigwa marufuku. Hata hivyo, Iran na Israel si wanachama wa mkataba huo.