Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Bw. Ashraf Suryaningrat, ameweka bayana kuwa mgodi huo utaendelea kushirikiana na Serikali katika vita dhidi ya Virusi vya Ukimwi ili kufanikisha malengo ya Sifuri Tatu (yaani hakuna maambukizi, hakuna unyanyapaa, na hakuna vifo kufikia mwaka 2030).
“Mgodi wa GGML sio tu unajihusisha na uchimbaji madini wenye uwajibikaji, bali pia unachangia maendeleo ya jamii kupitia sekta mbalimbali, ikiwemo afya — ambayo ni msingi mkuu wa maendeleo,” amesema.
Ameongeza kuwa upandaji wa Mlima Kilimanjaro haukuwa tu kielelezo cha utalii, bali pia ulikuwa kielezo cha na uzalendo ambapo waliopanda mlima huo, wakiwemo watoto yatima wawili wenye umri wa miaka 13 walijitolea kwa jasho na maumivu kwa ajili ya kuonesha uzalendo huo na upendo kwa jamii.
Akiongea mapema asubuhi wakati wa kuwapokea mashujaa hao, Pia Simon Shayo, Makamu wa Rais wa Uendelevu na Mahusiano, Africa, AngloGold Ashanti, kampuni mama ya GGML amesema katika kuadhimisha miaka 25 ya mgodi huo hapa nchini, wanaona fahari kampeni hiyo ikiendelea kufanyika kila mwaka kwa kipindi cha miaka 23 mfululizo, kuendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali na kuleta matokeo chanya katika jamii.
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kupitia kampeni hii katika miaka ijayo ili kufikia malengo yaliyowekwa,” amesema Bw.Shayo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Kiseo Nzowa, ameeleza kuwa mbali na upandaji wa Mlima Kilimanjaro, kampeni hiyo pia ilihusisha upimaji wa hiari wa UKIMWI na utoaji wa elimu ya kujikinga, ambapo jumla ya watu 1,632 walipimwa, nusu yao wakiwa wanawake, na kondomu 54,728 zilisambazwa.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita (Bw. Martin Shigela) uliopo mgodi huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Bi. Sakina Mohamed, ameongeza kuwa mgodi huo umechangia miradi mbalimbali ya kijamii mkoani humo — ikiwemo maji, ujenzi wa barabara na kulea kituo cha watoto yatima — kama sehemu ya kuunga mikono juhudi za Serikali.
Wakati wa makabidhiano hayo ya vyeti kwa washiriki, kampeni hiyo pia ilikabidhi zaidi ya milioni 130 kwa asasi tano za kiraia wakati wa sherehe hizo zilizofanyika Moshi Club mkoani humo. Taasisi zilizokabidhiwa fedha ni pamoja na Mtandao wa Vijana wanaoishi na Virusi vya Ukimwi ( Network For Young People Living with HIV, ambao wamekabidhiwa kiasi cha shilingi milioni 29.
Taasisi nyingine ni Pata Maendeleo ya Rukwa iliyokabidhiwa milioni 20, Kikundi cha Wanawake cha Kupambana na Ukimwi cha Kilimanjaro (KiwakkukiI kilichokabidhiwa milioni 29 , Jali Afya Yako, Epuka Maambukizi kilichokabidhiwa milioni 30 na Kongwa Arusha DC kilichokabidhiwa kiasi hicho hicho cha fedha. Kampeni ya GGM Kili Challenge iliyoanza miaka 23 iliyopita, imekuwa ikikusanya fedha kwa ajili ya kusaidia katika mapambano ya janga hilo kupitia taasisi mbalimbali zilizojikita katika mapambano hayo na kutoa misaada katika hospitali, vituo vya afya na kulelea watoto yatima. |
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii