Makubaliano kati ya M23 na serikali ya Congo kuanza kutekelezwa wiki hii

Makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, yanatarajiwa kuanza kutekelezwa wiki hii.

Kwa wataalamu wa masuala ya siasa na usalama wa eneo la maziwa makuu, wanasema wiki hii ni muhimu kwa pande zote zinazohusika kwenye mgororo wa mashariki mwa Congo, ambapo itajulikana ikiwa zitaheshimu kile walichokubaliana Doha, Qatar.

Makubaliano haya yaliyotiwa saini Julai 19 huko Doha, Qatar, yalishuhudia pande husika zikikubaliana kimsingi "kusitisha mapigano” na "kuendeleza majadiliano" ili kuwezesha kurejea "kwa hiari" kwa wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao.

Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanatahadharisha kuwa, mchakato wa amani katika eneo hilo lenye utajiri wa madini bado uko mashakani na hauna uungwaji mkono wa kutosha toka jumuiya ya kimataifa.

Mamia ya watu walifariki katika mapigano wakati waasi hao wakiuchukua mji wa Goma na Bukavu, huku maelfu wakiyakimbia makazi yao, wakati huu taifa hilo likishuhudia janga baya zaidi la kibinadamu duniani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii