Nigeria yadhoofika kimataifa kutokana na kutokuwa na mabalozi

Nigeria iko chini ya shinikizo la kidiplomasia kutoka Marekani na Falme za Kiarabu, ambazo zimeweka vikwazo vikali kwa upataji visa kwa raia wake wiki iliyopita. Siku ya Jumanne, Julai 15, Rais Bola Tinubu alitangaza  kwamba majadiliano ya "kidiplomasia" yataanzishwa kuhusu suala hilo, isipokuwa tu kwamba, kuna tatizo, Nigeria haina tena balozi popote duniani isipokuwa New York na Geneva.

Alipoingia madarakani, Rais Bola Tinubu aliwarejesha nyumbani mabalozi 109 kote ulimwenguni. Ilikuwa mwezi Septemba 2023, na hakuna uteuzi mpya ambao umefanywa tangu wakati huo. Hali hii inadhoofisha na kuitenga Nigeria katika ulingo wa kimataifa.

Rais Bola Tinubu hakutoa maelezo yoyote alipowaita mabalozi na makamishna wakuu wa Nigeria waliokuwa wakihudumu nje ya nchi mnamo mwezi Septemba 2023, isipokuwa wawakilishi wake wa kudumu huko New York na Geneva.

Suala hilo lilipoanza kuibua wasiwasi wa umma, Waziri wa Mambo ya Nje alitoa maelezo kadhaa: mwanzoni mwa muhula wake, mkuu mpya wa nchi, mwenye shughuli nyingi na mageuzi yake ya kiuchumi, hakuwa na wakati wa kufanya uteuzi mpya.

Kisha waziri akapendekeza tatizo la kifedha: Nigeria inatatizika kutafuta fedha za kufadhili misheni yake ya kidiplomasia. Hoja hii inahatarisha kuharibu zaidi taswira ya nchi kimataifa, kulingana na baadhi ya waangalizi.

Kutokuwepo kwa wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Nigeria katika ngazi ya kimataifa ni tatizo kubwa kwa baadhi ya mazungumzo ya kimkakati na majadiliano ya nchi mbili. Maafisa, katika Wizara ya mambo ya Nje wanokaimu katika masuala ya kidiplomasia, pia hawana hadhi inayofaa ya kuingiliana na mamlaka ya kisiasa ya nchi mwenyeji.

Mnamo mwezi Aprili 2025, orodha ya mabalozi watarajiwa iliripotiwa kuwasilishwa kwa uchunguzi wa ndani wa usalama, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Nigeria, lakini kwa mara nyingine tena, ofisi ya rais ilikaa kimya, na hakuna uteuzi rasmi uliofanywa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii