Wastaafu wameridhishwa na dira ya taifa 2050

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete amepongeza uzinduzi wa Dira 2050 akisema kuwa ni hatua kubwa katika historia ya maendeleo ya nchi na kwamba wastaafu, akiwemo yeye, wameridhika na dira hiyo, huku akimtupia kijembe cha utani aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Kikwete ameyasema hayo leo Alhamisi Julai 17, 2025 katika hafla ya uzinduzi wa Dira hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma mgeni rasmi akiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mheshimiwa Rais, kwa jinsi mambo yalivyofanyika, sisi wastaafu tunasema hongera sana. Umefanya jambo kubwa kwa historia na maendeleo ya nchi yetu, jambo ambalo litafanya jina lako liendelee kutajwa kwa miaka 25 ijayo. Hongera sana Profesa Kitila Mkumbo. Sisi wastaafu tumeridhika, tumefurahi na kufarijika kwamba umeendesha mambo kiprofesa hasa,” amesema Kikwete.

Katika hatua nyingine Kikwete amegusia historia ya kisiasa ya Profesa Kitila akisema:“Lakini labda niseme kitu kimoja, unajua huyu pengine aliteleza tu. Huyu Kitila Mkumbo alikuwa Mwenyekiti wa Vijana wa CCM Mkoa wa Singida, sijui Mbowe (Freeman Mbowe) alikuja kumdanganya nini yule pale. Kwa hiyo haya anayoyafanya sasa ni ya ki-CCM. CCM anakumbuka kule alikotokea.”


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii