Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, sasa ameitaka serikali yake kuimarisha mahitaji ya viza kwa wanadiplomasia wa Algeria ambapo wakati huu mzozo baina ya rai hao wa Algiers kuhusu kufukuzwa umeonekana ukiendelea kushika kasi nchini humo.
Katika barua yake kwenda kwa Waziri Mkuu, Francois Bayrou, Macron amesema matatizo yanayoongezeka ambayo Ufaransa inakabiliana nayo katika suala la uhamiaji na usalama na nchi ya Algeria yanahitaji msimamo mkali zaidi dhidi ya koloni lake la zamani.
Aidha alimuagiza waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, aziombe nchi za eneo la Schengen -- ambazo zinaruhusu safiri bila pasi ya kusafiria kati ya mipaka yao -- kusaidia Ufaransa kwa kutumia sera kali ya viza, haswa kwa utoaji wa viza za muda mfupi kwa maafisa wa Algeria wanaohusika na pasipoti zilizojumuishwa katika makubaliano ya 2013.
Uhusiano kati ya Paris na Algiers umezorota tangu Julai 2024 baada ya Ufaransa kutangaza kutambua mamlaka ya Morocco kuhusu eneo linalozozaniwa la Sahara Magharibi, ambalo Rabat inataka jumuiya ya kimataifa itambue kuwa sehemu yake.
Mvutano uliongezeka baada ya Algeria kumzuia mwandishi Boualem Sansal mwenye uraia wa nchi hizo mbili mwezi Novemba, lakini ukafikia pabaya zaidi mwezi Februari mwaka huu wakati raia wa Algeria ambaye Ufaransa ilijaribu kwa muda mrefu kumrejesha nyumbani kukamatwa akituhumiwa kwa shambulio la kisu katika mji wa Mulhouse.