Shirika moja la kimataifa linalohamasisha masuala ya uzazi wa mpango, IPPF, sasa linasema nchi ya Marekani kuchoma moto wa dawa za vidhibiti mimba zenye thamani ya dola za Marekani milioni 9.7 kutasababisha mimba laki 1 na elfu 74 zisizotarajiwa na utoaji mimba elfu 56 usio salama.
Mataifa ya DRC, Kenya, Tanzania, Zambia na Mali yalikuwa yameratibiwa kupokea dawa hizo, hali inayotishia kusababisha matokeo laki 1 na elfu 74 ya mimba zisizotarajiwa na uaviaji Elfu 56 wa mimba hizo.
Vidonge hivyo tayari vilikuwa vinasubiri kusambazwa katika mataifa husika kabla ya serikali ya Marekani kuzuia mpango huo licha ya kwamba muda wa matumizi ya dawa hizo haukuwa umepita.
Mwezi uliopita, Washington ilisema uamuzi wa kuharibu dawa hizo ulikuwa umeafikiwa baada ya kukosekana kwa mnunuzi aliyeafikia vigezo.
Kwa mujibu wa Marekani, sheria zake haziruhusu kutuma misaada kwa mashirika yanayouunga mkono uuaviaji mimba.