KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka amesema serikali inaboresha utaratibu wa utumishi wa umma kwamba ili mtumishi apande daraja au athibitishwe kazini atalazimika kufanya mtihani kupima uwezo wake.
Aidha amewataka watendaji kuacha tabia ya kuwakataa watumishi wanaohamishiwa kwenye taasisi zao au kutaka kuwahamisha.
Ameonya pia kwamba watumishi wenye changamoto au matatizo ya kiutendaji wasihamishiwe kwenye taasisi nyingine bali wabaki katika taasisi walizopo na kuadhibiwa ndani ya taasisi husika.
Alitoa kauli hiyo juzi katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani wakati akifungua mafunzo ya siku nne kwa watendaji wakuu wa taasisi za umma 114 yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi.
Balozi Kusiluka alisema mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo watendaji hao na kuwapa fursa ya kubainisha changamoto, jinsi ya kuzishughulikia na kuishauri serikali.