Wanajeshi wasiopunguwa watatu wa Ukraine wameuawa na kumi na wanane kujeruhiwa katika shambulio la Urusi siku ya Jumanne, Julai 29, dhidi ya kambi ya mafunzo ya kijeshi, jeshi la Ukraine limetangaza.
Mashambulizi haya yanajiri huku Rais wa Marekani Donald Trump akimpa mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, siku kumi kuanzia Jumanne kumaliza mzozo huo, la sivyo atakabiliwa na vikwazo kutoka kwa Marekani.
"Adui amezindua shambulio la kombora kwenye eneo la moja ya vitengo vya mafunzo vya vikosi vya ardhini," jeshi la ardhini la Ukraine limesema kwenye Facebook. "Wanajeshi watatu wameuawa na 18 kujeruhiwa," limeongeza, bila kutaja ambapo shambulio hilo lilitokea.
Siku ya Jumanne, Urusi ilirusha "makombora sita" na kufanya "mashambulio 1,229" kwa kutumia ndege zisizo na rubani zinazojilipua, jeshi limesema.
Wakati wa usiku uliotangulia, angalau raia 25, ikiwa ni pamoja na mwanamke mjamzito na watu wapatao 15 waliozuiliwa jela katika eneo la kusini la Zaporizhzhia, waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Urusi, kulingana na mamlaka, ambayo imeripoti zaidi ya watu 70 waliojeruhiwa.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameshutumu shambulizi dhidi ya gereza hilo, na kuliita "shambulio la kimakusudi lililotekelezwa kwa nia mbaya," akisisitiza kwamba "Urusi haikuweza kujua kwamba ilikuwa wakiwalenga raia." Watu 16 waliuawa na 43 walijeruhiwa katika shambulio hilo, kulingana na utawala wa mkoa.
Kremlin kupitia msemaji wake, Dmitry Peskov, imekanusha kuwalenga "raia," ikisema kuwa jeshi la Urusi limetekeleza milipuko ya mabomu "kwenye miundombinu ya kijeshi."
Jeshi la Wanahewa la Ukraine limeeleza kuwa lilikumbana na makombora mawili na ndege zisizo na rubani 37 mara moja kutoka Jumatatu hadi Jumanne, 32 kati ya hizo zilidunguliwa. Idadi hii ni ndogo kuliko kawaida, kwani Urusi imezidisha mashambulizi yake katika miezi ya hivi karibuni, yenye uwezo wa kurusha zaidi ya makombora 500 kila usiku.
Mashambulizi mengine ya Urusi yamesababisha vifo vya watu sita katika mkoa wa Kharkiv (kaskazini mashariki), mamlaka imesema. Mji wa Kharviv umelengwa tena alfajiri ya Jumatano na shambulio la ndege isiyo na rubani, kulingana na Meya Igor Terekhov.
"Putin anakataa usitishaji vita, anaepuka mkutano wa viongozi, na kuongeza muda wa vita," Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiga alisema siku ya Jumanne, akitaka Urusi kunyimwa "bajeti yake ya vita."
Kwa upande wake, Donald Trump aliongeza shinikizo kwa kufafanua uamuzi wake wa mwisho kwa Vladimir Putin: Putin ana siku kumi-kuanzia Jumanne-kumaliza vita vilivyoanzishwa na uvamizi wa Urusi kwa Ukraine mnamo mwezi wa Februari 2022. Vinginevyo, Marekani itaweka vikwazo kwa Moscow, "ushuru, na mambo mengine."
"Hakuna sababu ya kusubiri. Hatuoni maendeleo yoyote," rais wa Marekani alibainisha siku ya Jumatatu, baada ya awali kupendelea chaguo la mazungumzo, lakini kwa matokeo machache sana.