Kituo cha EALC kuzinduliwa Agosti mosi

Leo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila, amefanya mkutano na waandishi wa habari katika hoteli ya Johari Rotana, ambapo ametangaza rasmi uzinduzi wa Kituo cha East Africa Logistic Center kilichopo Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika tarehe 1 Agosti, 2025, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Rais atazindua kituo hicho kwa lengo la kuleta mapinduzi makubwa ya kibiashara na uwekezaji wa kimkakati nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mh. Chalamila, ujenzi wa kituo hicho umegharimu zaidi ya dola milioni mia moja za Kimarekani (USD 100M). Kituo hicho kitakuwa mhimili mkubwa wa shughuli za kibiashara, usambazaji na uwekezaji, kikilenga kurahisisha mnyororo wa usambazaji wa bidhaa na huduma ndani na nje ya Tanzania.

Mheshimiwa Chalamila ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huo na kuchangamkia fursa lukuki zitakazotokana na uwepo wa kituo hicho.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii