Mmomonyoko wa maadili chanzo kukithiri rushwa serikalini

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Crispin Chalamila, amesema kuwa kukosekana kwa maadili katika ngazi ya familia ndiyo chanzo cha kukithiri kwa rushwa kwa watumishi serikalini na sehemu nyingine zote.

Chalamila, amesema hayo leo Julai 30, 2025 jijini Dodoma, wakati alipokuwa akifungua kikao kazi cha siku mbili cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora baina ya taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka simazi za maadili ya kitaaluma.

”Kaulimbiu ya kikao hiki inasema, ”Mmomonyoko wa maadili ni chanzo kimojawapo cha rushwa, tushirikiane kuimarisha maadili”, tumechagua kuitumia kaulimbiu hii kutokana na ukweli kwamba kukosekana kwa maadili ni mwanzo wa matatizo yote ikiwemo tatizo la Rushwa.

“Kukosekana kwa maadili katika ngazi ya familia ndiyo chanzo cha kukithiri kwa rushwa katika watumishi serikalini na sehemu nyingine zote,”amesema Chalamila

Vile vile, amesema kuwa mtumishi hata awe na weledi mkubwa kiasi gani kama hatokuwa na maadili mazuri basi ni lazima ataingia kwenye vitendo viovu ikiwamo kuomba rushwa ili atoe huduma kwa wanaoihitaji.

Kadhalika, amesema wajibu wa kusimamia maadili ya watumishi wa umma katika utumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kudhibiti uwepo wa vitendo vya Rushwa, ni suala mtambuka ambalo kisheria liko chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa mujibu wa kifungu cha 8(3)(e) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii