Wakorea wawanoa wanafunzi ATC Akili Unde

RAIA wa Jamhuri ya Korea Kusini, wametoa mafunzo ya matumizi ya Akili Unde (AI) kwa wanafunzi 50 wa Uhandisi wa Chuo cha Ufundi cha Arusha (ATC) kilichopo jijini hapa ili kuwajengea maarifa ya kutumia teknolojia katika taaluma yao .

Rai hao, wataalamu wabobezi katika teknilojia hiyo, wameunda kikundi cha kujitolea katika Teknolojia ya Habari (IT) cha Wakorea Kusini Ulimwenguni (WFK) na kutoa mafunzo hayo kwa siku nne katika chuo hicho kwa wanafunzi hao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa baada ya kuhitimisha kutoa mafunzo hayo, Kiongozi wa kikundi hicho kinachotambulika kwa jina la ‘Pamoja’ Donghun Lee, Mwalimu wa Darasa la IT alisema kuwa wametoa mafunzo hayo kwa msaada wa Wakala wa Kimataifa wa Habari (NIA), Taasisi ya Umma ya Korea Kusini na Shirika la kimataifa lisilokuwa la kiserikali la E3Mpower. 

Kwa mujibu wa Lee, elimu waliyopata wanafunzi hao, itawasaidia kupata uzoefu wa teknolojia ulimwenguni na kuitumia vizuri.

Alisema baadhi ya mambo waliyofundishwa wanafunzi hao ni Anuwai ya AI kutoka kwa dhana za msingi na uainishaji wa picha hadi usindikaji wa lugha asili (NLP), mashine na  matumizi ya vitendo ya teknolojia hiyo.

 Yoonkyo Cho, Mwalimu wa Lugha ya Kiingereza nchini humo, alisema wamekuja Tanzania kujitolea kufundisha na kutumia maarifa yao kuwasaidia wanafunzi hao kuwa wabunifu zaidi.

“Tanzania na Korea ni marafiki kwa muda mrefu, hivyo tunatumia urafiki wetu kuja hapa katika chuo chetu cha ufundi kufanya mpango wa uandishi wa AI kwa siku nne, kwa ufupi wamejifunza juu ya AI. Je! tunawezaje kutumia kwenye maisha yetu? Na tuko katika siku ya kwanza tunajifunza juu ya usindikaji wa lugha ya asili,” alisema Cho.

Mophat Gipson, mwanafunzi wa ATC katika kozi ya kompyuta sayansi, alisema mafunzo hayo yatawasaidia kupunguza muda wa kufanya kazi kwa kutumia programu mbalimbali za Akili Unde.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii