Thailand imeishutumu Cambodia leo Jumatano, Julai 30, kwa "ukiukaji wa wazi" wa usitishaji mapigano uliotekelezwa kati ya nchi hizo mbili jirani baada ya siku kadhaa za mapigano mabaya, ikidai kuwa wanajeshi wa Cambodia wameanzisha shambulio la usiku.
Bangkok na Phnom Penh walikubaliana kusitisha mapigano, ambao ulianza kutekelezwa siku ya Jumatatu usiku baada ya siku tano za makabiliano kwenye mpaka wao wa pamoja wenye urefu wa kilomita 800 katika ya mzozo wa eneo.
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Thailand imetangaza kwamba wanajeshi kadhaa wa Thailand katika mkoa wa mashariki wa Sisaket wameshambuliwa leo Jumatano asubuhi "na vikosi vya Cambodia" vilivyo na "silaha ndogo" na maguruneti.
"Hii inaonyesha ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano," Wizara ya Mambo ya Nje ya Thailand imesema katika taarifa. "Kitendo kama hicho cha uchokozi kinafanya tena ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano na vikosi vya Cambodia na ukosefu wao wa nia njema," chanzo hicho kimeongeza.
Msemaji wa serikali ya Thailand Jirayu Huangsab pia ameripoti mapigano ya usiku katika taarifa yake, akisema kwamba "upande wa Thailand umedumisha udhibiti wa hali" na kwamba hali ya jumla kwenye mpaka imekuwa "ya kawaida" tangu saa 2:00 asubuhi.
Siku ya Jumanne, jeshi la Thailand liliwashutumu wapinzani wake kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano katika maeneo mengi, madai ambayo yalikanushwa na Phnom Penh.
Chuki ya muda mrefu kati ya Thailand na Cambodia inahusishwa na mzozo wa eneo ulioanzia enzi za Indochina ya Ufaransa.