Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipango Miji (TPRB) imewataka wataalam wa mipangomiji na kampuni za upangaji miji nchini wenye sifa lakini hawajasajiliwa, kuhakikisha wanatuma maombi ya usajili kabla ya Septemba 23 mwaka huu.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Kaimu Msajili wa Bodi hiyo, TP. Martha Mkupasi, alipokuwa akieleza hali ya usajili wa wataalam na kampuni za upangaji miji nchini.
Amesema hadi kufikia Mei 2025, Bodi imefanikiwa kusajili wataalam 514 wa mipangomiji na kampuni 99 zinazotoa huduma za upangaji miji. Hata hivyo, bado wapo wataalam wenye sifa ambao hawajafanya usajili na wanapaswa kufanya hivyo kabla ya kikao cha usajili kinachotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Septemba.
“Napenda kuwataarifu wataalam wote wa mipangomiji wenye sifa ya kusajiliwa kuwa Bodi inategemea kufanya kikao cha kusajili wataalam na kampuni mwishoni mwa mwezi Septemba. Ni muhimu kuwasilisha maombi mapema ili tuweze kuyapitia na kutoa usajili,” amesema TP. Mkupasi.
Aidha, amesisitiza kuwa ni kinyume cha sheria kwa wataalam au kampuni kufanya kazi za upangaji miji bila kusajiliwa, huku akibainisha kuwa Bodi inaendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ili kuimarisha uelewa juu ya umuhimu wa usajili huo.
TP. Mkupasi ameongeza kuwa Bodi ya TPRB itaendelea kusimamia maadili na nidhamu ya wataalam wa mipangomiji, kutoa ushauri wa kitaalam pamoja na kuchunguza ukiukwaji wowote wa maadili katika sekta hiyo.