Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imewakumbusha waombaji wa mikopo na ufadhili wa Samia Scholarship kuwa dirisha la maombi kwa mwaka wa masomo 2025/2026 litafungwa rasmi Agosti 31 mwaka huu bila kuongezwa muda.
HESLB imetoa kauli hiyo jana Alhamisi Agosti 21 mwaka huu kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, ikiwataka wanafunzi wenye sifa kuhakikisha wanakamilisha maombi yao mapema kabla ya muda kuisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia, akizungumza na waandishi wa habari Agosti 11 mwaka huu alisisitiza kuwa dirisha la maombi lililofunguliwa Juni 15 mwaka huu halitaongezewa muda na litafungwa kama lilivyopangwa.
“Zimebaki siku 10 pekee, hivyo ni vyema wanafunzi wenye sifa kuhakikisha wanafanya maombi yao mapema ili kuepuka msongamano wa dakika za mwisho,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa msaada zaidi, wanafunzi wanashauriwa kutembelea tovuti rasmi ya HESLB.