Serikali imetangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa ulipaji fidia kwa wananchi wa Mitaa ya Nyakabale na Nyamalembo katika Halmashauri ya Manispaa ya Geita, ili kupisha shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML). Hatua inayoleta suluhu ya mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 26.
Akizungumza leo Agosti 21 mwaka huu Mkoani Geita, Waziri wa Madini, Mhe.Anthony Mavunde, amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikifuatilia kwa karibu changamoto za wananchi wa Geita na kutoa maelekezo mahsusi kuhakikisha zinatatuliwa kwa ufanisi.
Mhe. Mavunde amebainisha kuwa GGML wameridhia kuanza mchakato wa kuwalipa fidia wananchi wa eneo la Nyakabale na Nyamalembo kwa mujibu wa utaratibu ili kupisha shughuli za mgodi. Amesema kuanzia kesho Agosti 22 mwaka huu timu ya wataalamu wa Serikali itaanza kazi ya uthamini wa mali, na ndani ya siku 40 tathmini hiyo itakamilika ili wananchi waweze kulipwa stahiki zao.
Hata hivyo Waziri ameeleza kuwa, mgogoro huo ulikuwa na hoja 13 za msingi ambazo zilihitaji kushughulikiwa, ambapo ndani ya mwaka mmoja na miezi mitatu Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kutatua hoja 10 kati ya hizo na hatimaye leo kutatua hoja nyingine mbili.
Aidha Waziri Mavunde ameeleza kuwa, katika jitihada hizo, GGML imekubali kurekebisha mipaka yake ya leseni ya uchimbaji lna kuliachia eneo linalobaki kwa ajili ya wakazi wa maeneo hayo.
Pia, Waziri Mavunde ametumia nafasi hiyo kuwaonya na kuwakumbusha wananchi kuepuka tabia ya ‘tegesha’ kwani inaweza kukwamisha zoezi la tathmini na ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaostahili kupata haki zao kwa wakati na kuleta usumbufu kwa mwekezaji na wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigella amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kufuatilia kwa karibu mgogoro huo wa muda mrefu, na kumpongeza Waziri Mavunde kwa kusimamia utekelezaji kwa umakini.
Wananchi wanaotarajiwa kufanyiwa tathmini na kulipwa fidia ni wa mitaa ya Nyakabale na Nyamalembo ndani ya Manispaa ya Geita.