Wanaodhalilisha bendera ya Marekani kupewa adhabu kali

Rais wa Marekani, Donald Trump ametia saini amri ya kiutendaji (Executive Order), inayopiga marufuku kitendo cha kuchoma bendera ya nchi hiyo, akisema yeyote atakayefanya hivyo atakwenda jela mwaka mmoja bila msamaha.

Kwa mujibu wa CBS News, Al Jazeera na tovuti rasmi ya The White House wanaochoma bendera watafungwa mwaka mmoja na kuwekewa rekodi ya jinai.

Mwanasheria mkuu ameagizwa kuhakikisha kesi hizo zinashtakiwa kwa kiwango cha juu kabisa. Pia, kwa wageni watakaochoma bendera watapata adhabu ikiwemo kufutiwa viza na kufukuzwa nchini humo.

Tovuti ya The White House imesema hati hiyo ya amri ya rais iliyotiwa saini na Trump Agosti 25 mwaka huu inataka kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya vitendo hivyo vya kuchoma au kudhalilisha bendera ya Marekani.

Kwa ufupi, amri hiyo inamaanisha bendera ya Marekani inaelezwa kama alama takatifu ya taifa, uhuru na mshikamano wa Wamarekani.

Sasa kitendo cha kuichoma au kuidhalilisha kinachukuliwa kama cha dharau na chenye kuhamasisha vurugu.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii