Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mafia mkoani Pwani Salehe Kikweo amefariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Mji Handeni Mkoa wa Tanga.
Taarifa ya kifo hicho imetolewa na Katibu wa CCM Wilaya ya Handeni Mayassa Kimbau leo Jumanne Agosti 26 mwaka huu kupitia mitandao ya kijamii na kueleza Kikweo amefariki dunia asubuhi ya leo hospitalini hapo na mwili wake umehifadhia hapohapo.
Amesema taarifa zaidi kuhusu wapi yatafanyika mazishi yake itatolewa baadaye baada ya familia na viongozi wengine kukutana ili kupanga taratibu vizuri. Kikweo ni mwenyeji wa Handeni.
"Nimepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa ya msiba wa ndugu yetu kaka yetu mpendwa Kikweo aliyefariki asubuhi hii ya leo na mwili umehifadhiwa Hospitali ya Bomani mipango ya mazishi inaendelea kufanyika," imeeleza taarifa hiyo.
Akizungumzia msiba huo Mwenyekiti wa CCM, wilayani Handeni Amiri Changogo ambaye ni mmoja wa viongozi aliyefanya kazi na katibu huyo kwa muda, amesema kifo cha Kikweo kimetokea ghafla na wala hajaugua.