KUELEKEA KATIKA KIPINDI CHA UCHAGUZI KURA ni nyenzo muhimu zaidi ya mwananchi katika kuimarisha na kuwezesha demokrasia imara.
Kupiga kura si wajibu wa kikatiba pekee, bali ni haki ya msingi inayompa kila raia nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika maamuzi ya mustakabali wa taifa lake. Kupitia kura, wananchi huamua ni viongozi gani watawaongoza na sera zipi zitakazotekelezwa kwa miaka inayofuata.
Hali hiyo huongeza uwajibikaji wa viongozi kwa kuwa wanatambua kuwa madaraka yao yanatokana na ridhaa ya wananchi. Faida kubwa ya kupiga kura ni kuhakikisha sauti ya kila mtu inahesabiwa. Hata kura moja inaweza kuleta mabadiliko katika kushinda au kushindwa kwa mgombea, hasa katika maeneo yenye ushindani mkubwa.
Kupiga kura kunawapa wananchi nguvu ya kuondoa viongozi wasiofaa na kuwachagua wale wanaoaminika kutekeleza ahadi na kulinda maslahi ya umma. Kura pia huimarisha uwakilishi wa wananchi bungeni, kwenye mabaraza ya madiwani, na kwenye ofisi za juu za utendaji.
Kadri wananchi wanavyoshiriki kwa wingi, ndivyo inavyoongeza uhalali wa serikali na kuimarisha misingi ya utawala bora. Aidha, kura huimarisha mshikamano wa kitaifa kwa kuwa mchakato wa uchaguzi ni jukwaa la amani la kushindana kwa hoja na sera, badala ya mabavu au migongano.
Wananchi Zingatieni sheria za kupiga kura – NEC
Kura huchochea uwajibikaji kwa viongozi waliopo madarakani, kwa kuwa wanatambua kura za wananchi ndizo zitakazobaini hatima yao kisiasa. Kupuuza haki ya kupiga kura ni kuruhusu wengine wafanye maamuzi kwa niaba yako, jambo linaloweza kusababisha kupoteza fursa ya kuchangia mabadiliko unayoyataka.
Hivyo, kila mwananchi anayepiga kura anachangia moja kwa moja katika kujenga taifa lenye demokrasia imara, viongozi bora, na maendeleo endelevu yanayoheshimu matakwa ya watu wake. Mwananchi atambue kuwa kura ni dhamana na haki ya msingi ya kila mwananchi aliye na sifa za kupiga kura kama ambavyo zimeainishwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Kwa wasiofahamu, karatasi ya kupigia kura iko kama karatasi zingine isipokuwa inakuwa na thamani kubwa hasa wakati inapokwenda kutumbukizwa kwenye sanduku la kupigia kura. Kura inapotumbukizwa tu kwenye sanduku la kura hugeuka na kuwa chombo kizito na chenye thamani kubwa kinachoenda kuwaweka viongozi madarakani na kwa wakati huo haiitwi karatasi tena.
Ni kitu chenye thamani kwa sababu ndicho huenda kufanya maamuzi ya mgombea yupi kutoka chama kipi cha siasa anayefaa kuchaguliwa kuwaongoza wananchi. Hivyo basi wananchi watambue umuhimu wa karatasi (shahada) walizo nazo za kupigia kura.
Kuacha kutoenda kupiga kura kwanza hakumuondolei mtu matatizo aliyo nayo kama ya watu wengine. Lakini pili kwa kukosekana kwa kura yake moja inaweza kuifanya nchi ikawapata viongozi wabovu.
Suluhisho la kuondokana na changamoto zinazowakabili wananchi si kwa wao kutoshiriki katika kupiga kura na kuwachagua viongozi, bali wanatakiwa washiriki kupiga kura ili wawapate viongozi makini watakaoweza kushughulikia changamoto walizo nazo.
Wajibu wa mpigakura Katika uchaguzi wa mwaka huu, kwa mujibu wa INEC anachotakiwa kufanya mpigakura ni kuwahi asubuhi kwenye kituo cha kupigia kura na kufuata taratibu za INEC kwa kujipanga kwenye mstari na akiwa na shahada yake na kuingia kwenye chumba maalumu cha kupigia kura.
Mpigakura atapaswa kupiga kura kwa siri kwa kuweka alama ya vema katika kisanduku cha mgombea anayemtaka kwa kufauta utaratibu ulioelekezwa. Mpigakura anapaswa kuwa makini anapoweka alama ya vema kwenye kisanduku kwa kuwa ikitoka nje ya kisanduku aua akaweka alama hiyo juu ya picha ya mgombea kura yake itakuwa imeharibika.
Akishamaliza kuweka alama ya vema anatakiwa aikunje karatasi yake mara mbili kisha aitumbukize kwenye sanduku la kura, lakini ni lazima ahakikishe anatumbukiza kura katika sanduku sahihi kulingana na nafasi anayopigia kura iwe ni Rais, Mbunge au Diwani.
Kwa mujibu wa INEC kituo cha kupigia kura kwa ni lazima kibandikwe bango la kutambulisha kuwa ni kituo cha kupiga kura na kinapaswa kufunguliwa saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni. Kama mpigakura hakutendewa haki wakati wa kupiga kura anatakiwa kusajili malalamiko yake kwenye fomu maalumu ambayo hupatikana kwenye vituo vyote vya kupigia kura.
Haki ya kupiga kura Kila raia wa Tanzania aliye na shahada ya kupiga kura ana haki ya kupiga kura. Mtu asikubali kubaguliwa kutopiga kura kwa sababu ya dini yake, rangi yake au maumbile yake au kwa namna yoyote ile ya kupewa vitisho.
Uchaguzi huu ni muhimu kwa sababu ndio utakaoamua serikali ijayo na hatma ya maendeleo ya nchi kwa miaka mitano ijayo. Matokeo Baada ya kupiga kura, zitahesabiwa kwenye vituo na matokeo yatabandikwa nje ya mbao za matangazo kwenye vituo hivyo.
Hapa wasimamizi wa uchaguzi watatangaza matokeo ya jumla ya ubunge na udiwani isipokuwa matokeo ya jumla ya urais yatatangazwa na INEC. Hayo hufanyika baada ya uhakiki wa idadi ya wapiga kura kulinganisha na idadi ya karatasi zilizotumika na idadi ya karatasi ambazo hazikutumika kisha kutoa taarifa kwa tume.
Hayo yote hufanyika kwa kufuata miongozo, sheria na kanuni ili mchakato mzima ukamilike kwa amani na
utulivu.