KATIBU Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewataka watendaji wa Tume ya Madini kuimarisha usalama kwenye migodi ya madini kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara sambamba na kutoa elimu ili kuepusha ajali zinazoweza kutokea na kusababisha vifo kwa wachimbaji wa madini.
Mhandisi Samamba ametoa agizo hilo leo Agosti 27 mwaka huu kwenye kikao kilichofanyika kwa njia ya mtandao kilichoshirikisha watendaji wa Tume ya Madini wakiwemo Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dk Janet Lekashingo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, Wakurugenzi na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ikiwa ni sehemu ya kuweka mikakati ya kuimarisha usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini nchini.
“Tunapoelekea katika msimu wa mvua za vuli ni vyema Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa zikaimarisha kaguzi kwenye migodi ya wachimbaji wadogo wa madini na kutoa elimu ya namna bora ya uchimbaji salama, pamoja na kuhakikisha wachimbaji wadogo wanavaa vifaa kinga kwenye shughuli za uchimbaji wa madini,” amesisitiza Mhandisi Samamba.
Katika hatua nyingine Mhandisi Samamba amewataka watendaji hao kusimamia afya za wachimbaji wa madini kwa kuhakikisha wanapimwa lengo likiwa ni kuhakikisha wanafanya kazi wakiwa na afya bora.
Aidha, amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kutatua migogoro kwa wakati kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kuongeza kuwa Wizara ipo tayari kusaidia pale itakapowezekana lengo likiwa ni kuhakikisha wachimbaji wa madini wanaendesha shughuli zao kwa amani.
Pia amewataka watendaji wa Tume ya Madini kuongeza kasi ya utoaji wa leseni za madini ili wachimbaji wa madini waanze kuchimba mara moja na kunufaika na rasilimali za madini.
“Ni vyema huduma za utoaji wa leseni za madini zikaendelea kuboreshwa sambamba na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanawapigia waombaji wa leseni kuchukua leseni zao ambazo zimeshatoka tayari badala ya kusubiri waombaji wazifuate ofisini,” amesema Mhandisi Samamba.
Amesema pia ni vyema maafisa Madini Wakazi wa mikoa wakashirikiana kwa karibu na Ofisi za Wakuu wa Mikoa.