Tanzania imeingia makubaliano na nchi zakimataifa dhidi ya dawa za kulevya

 TANZANIA imeingia makubaliano ya kimataifa na nchi zinazozalisha kwa wingi kemikali bashirifu ili kudhibiti matumizi yake katika utengenezaji wa dawa za kulevya.

Makubaliano hayo yaliafikiwa kupitia ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa 39 wa Kimataifa wa Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya (IDEC39), uliofanyika jijini Nashville, Marekani, chini ya uratibu wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya ya Marekani (DEA).

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, aliiongoza timu ya Tanzania na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni ushahidi wa jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha diplomasia ya kimataifa.

Pia Tanzania ilipata fursa ya kujadiliana na mataifa yanayozalisha mmea wa Kratom, ambao hutumika kutengeneza dawa hatari aina ya Mitragyna Speciosa, na kukubaliana namna bora ya kushirikiana kudhibiti usambazaji wake. 

Aidha, kupitia mikutano ya kimkakati na majadiliano ya kitaalamu, Tanzania imenufaika kwa kupata ushirikiano mpya na mashirika makubwa ya kimataifa, ikiwemo INL na mamlaka za udhibiti kutoka mataifa mengine barani Afrika.

Hatua hiyo imeimarisha mshikamano wa kimataifa katika kudhibiti mitandao ya dawa za kulevya, huku ikionyesha dhamira ya Taifa kulinda afya za Watanzania, kuimarisha usalama wa mipaka na kushirikisha vijana ipasavyo katika maendeleo ya Taifa kuelekea Dira ya Maendeleo 2050.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii