CCM Ilani ya imezingatia maudhui Dira ya maendeleo 2050

MGOMBEA Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuanza kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Mgombea huyo ameeleza ilani hiyo imezingatia maudhui na vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“CCM inaunga mkono matarajio yote yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na tunaahidi kuyatekeleza kikamilifu,” ameeleza Samia.

Ameeleza katika miaka mitano ijayo (2025-2030) CCM itaisimamia serikali kuhakikisha taifa linaendelea kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani; kulinda amani usalama na utulivu na kuimarisha ustawi wa Watanzania kwa kuwawezesha kiuchumi na kufungua fursa zaidi za ajira na biashara.

Samia ameeleza ilani hiyo ni ahadi ya CCM kwa Watanzania kuhusu hatua watakazochukua katika miaka mitano ijayo ili kuendelea kukuza uchumi na kipato cha wananchi, kuinua hali za maisha ya Watanzania wote, kuimarisha ustawi wa jamii, kulinda amani, usalama na utulivu katika nchi na kudumisha demokrasia na utawala bora.

“Kwa niaba ya CCM na serikali yake, ninawashukuru sana Watanzania wote kwa imani kubwa mliyotupatia kupitia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 uliotupatia uhalali wa kuunda serikali,” alieleza.

Samia ameeleza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na katika kipindi chote cha uongozi wake CCM imeendelea kusimamia mageuzi ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

“Ninawaahidi kuwa tutaendelea na mageuzi haya kwa lengo la kutokomeza umasikini, kuinua hali za maisha ya Watanzania wote na kuinua ustawi wa jamii na taifa letu,” alieleza.

Aliongeza: “Ninaomba muendelee kuiamini CCM na kuwachagua wagombea wake wote kwa nafasi za Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Urais wa Zanzibar, ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani”.

Samia ameishukuru CCM kwa kumteua awe mgombea wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumteua Dk Hussein Mwinyi awe mgombea wa kiti cha Urais wa Zanzibar.

“Ninaomba kura zenu za ndiyo kwangu binafsi nikiwa Mgombea kwa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk Hussein Ali Mwinyi kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar na wagombea wote wa CCM katika nafasi za ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani,” alieleza.

Samia anaweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kugombea Urais wa Tanzania kupitia CCM.

Awali aliweka historia ya kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke na baadaye akawa Rais wa kwanza
mwanamke wa Tanzania.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii