Ujumbe wa Ukraine utakutana na maafisa wa Marekani mjini New York Ijumaa

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametangaza siku ya Jumatano kwamba wajumbe wa utawala wake watakutana na maafisa wa Marekani mjini New York siku ya Ijumaa kama sehemu ya juhudi za kumaliza vita na Urusi.

Mjumbe maalum wa Rais wa Marekani Donald Trump, Steve Witkoff, awali aliambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba atakutana na maafisa wa Ukraine wiki hii.

"Siku ya Ijumaa, mikutano itafanyika New York, Marekani, na timu ya Rais Trump," baada ya "mikutano nchini Uswisi" siku ya Alhamisi, Zelensky amesema katika hotuba yake ya kila siku kwenye mitandao ya kijamii.

Kulingana na Zelensky, mkurugenzi mkuu katika ofisi yake, Andriy Yermak, na Waziri wa zamani wa Ulinzi Rustem Umerov walishiriki katika mazungumzo ya upatanishi nchini Qatar siku ya Jumanne, na mikutano zaidi imefanyika Saudi Arabia siku ya Jumatano.

Juhudi za kidiplomasia za kumaliza vita zimeongezeka katika wiki za hivi karibuni, kufuatia mkutano wa kilele kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na Trump huko Alaska, na kufuatiwa na mkutano wa Washington kati ya Trump na Zelensky, akiandamana na washirika wake wa Ulaya.

Trump amesema anataka kuandaa mkutano wa ana kwa ana kati ya marais wa Urusi na Ukraine, lakini mazungumzo yamepiga hatua kidogo, huku Moscow na Kyiv zikilaumiana kwa mkwamo huo.

Kabla ya kufikia makubaliano ya amani, Ukraine inataka hakikisho la usalama kutoka nchi za Magharibi ili kuzuia mashambulizi yoyote zaidi ya Urusi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii