SERIKALI ya Brazil imezindua mpango wa kuyaunga mkono makampuni ya ndani yaliyoathiriwa na ushuru wa asilimia 50 uliotangazwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa bidhaa kadhaa kutoka nchini humo.
Rais wa Brazil, Luiz InĂ¡cio Lula da Silva, amesema mpango huo wa kifedha wenye thamani ya dola bilioni 5.5 ni hatua ya awali ya kuwasaidia wauzaji wa bidhaa za ndani.
Kiongozi huyo wa mrengo wa kushoto, ambaye ushawishi wake umeongezeka tangu ushuru huo kutangazwa, amesema hajawahi kuzungumza na Trump na kudai kuwa rais huyo wa Marekani hana nia ya kufanya mazungumzo naye.
Mpango huo unatoa muda wa ziada wa ulipaji kodi kwa kampuni zilizoathirika na ushuru wa Marekani, mikopo kwa makampuni madogo na ya kati hadi mwisho wa mwaka 2026, pamoja na bima kwa bidhaa ambazo tayari zimeagizwa.