Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita, imewakamata wajumbe wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kata ya Nyankumbu Jimbo la Geita mjini walionekana katika picha mjongeo wakigawana rushwa katika mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM huku taasisi hiyo ikiendelea na uchunguzi kwa watia nia ngazi ya ubunge na udiwani wanaodaiwa kusambaza rushwa ya fedha kwa wajumbe ili wapate nafasi ya kuchaguliwa ili kugombea nafasi za ubunge na udiwani katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Tukio hili lilitokea tarehe 2 Agosti mwaka huu baada ya picha za video kuonyesha wajumbe wakigawana fedha kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa taarifa ya TAKUKURU, baada ya tukio hilo kusambaa, ofisi ya mkoa ilichukua hatua ya haraka kwa kuwatambua na kuwakamata wajumbe waliokuwa wakionekana kwenye picha hizo na kwamba Inadaiwa kuwa vitendo hivyo vilifanyika mara baada ya zoezi la kuwanadi wagombea ubunge kukamilika.
Katika tukio jingine, tarehe 4 Agosti mwaka huu TAKUKURU ilipokea taarifa kuwa chakula na vinywaji vilitolewa kwa wajumbe siku ya upigaji kura za maoni katika jimbo la Chato Kaskazini, picha za tukio hilo zilisambazwa pia kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha TAKUKURU kuanza msako na kuwakamata washukiwa kwa ajili ya mahojiano.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita James Ruge, amesema kuwa kutokana na matukio haya na mengine, ofisi imeanzisha uchunguzi unaoelekea kukamilika, ikiwa ni hatua ya kukusanya ushahidi ili kuthibitisha tuhuma za rushwa dhidi ya wahusika.